Yanga yaona mwezi
Jesca Nangawe
MABINGWA watetezi, Yanga jana walipata ushindi wao wa kwanza kwenye Ligi Kuu baada ya kuichapa African Lyon kwa mabao 2-1 katika mchezo uliofanyika kwenye Uwanja wa Azam, Chamazi jijini Dar es Salaam.
Mashabiki wa Yanga waliokuwa na hamu ya kuona timu yao ikishinda
mchezo huo walisubiri kwa dakika 35, mpaka mshambuliaji wa kimataifa wa
zamani wa Zambia, Davies Mwape alipofunga bao la kuongoza, lakini Lyon
walisawazisha bao hilo kupitia kwa Hamis Shengo kabla ya Rashid Gumbo wa
Yanga aliyeingia akitokea benchi kufunga bao la ushindi katika dakika
ya 63.MABINGWA watetezi, Yanga jana walipata ushindi wao wa kwanza kwenye Ligi Kuu baada ya kuichapa African Lyon kwa mabao 2-1 katika mchezo uliofanyika kwenye Uwanja wa Azam, Chamazi jijini Dar es Salaam.
Kwa matokeo hayo Yanga imejinasua mkiani kwa kufikisha pointi sita katika michezo mitano na kurudisha faraja kwa mashabiki wao kabla ya mechi ya Jumapili dhidi ya Azam itakayofanyika kwenye Uwanja wa Taifa.
Pamoja na rekodi mbaya ya utovu wa nidhamu kwa timu za Ligi Kuu msimu huu jana mwamuzi Mathew Akrama wa Mwanza alichezesha mechi bila ya kuonyesha kadi kwa mchezaji yeyote.
Mchezo ulianza kwa kasi na katika dakika ya 4, Sino Agustino alifanikiwa kuunganisha vizuri krosi ya Seleman Kassim, lakini shuti lake liligonga mwamba na kurudi uwanjani.
Yanga ilijibu mapigo katika dakika ya 10 na 14 kupitia kwa Mwape aliyeshindwa kumalizia nafasi mbili baada ya kupigiwa pasi nzuri na Nurdin Bakari na Shamte.
Bao la kwanza la Yanga lilipatikana baada ya Pius Kisambale kupiga pasi ndefu kutoka katikati ya uwanja ambayo ilitua kwa Shamte Ally aliyemtengenezea nafasi Mwape ambaye aliusukuma mpira wavuni katika dakika ya 35 na kuamsha shangwe kwa wanajangwani.
Dakika tano baadaye, Kassim wa Lyon aliwatoka mabeki wa Yanga na kipa Berko na kupiga shuti golini, lakini Juma Seif alifanya kazi ya ziada kuwahi mpira huo na kuutoa nje.Ikiwa inaonekana timu hizo zitaenda mapumziko huku Yanga ikiongoza kwa bao moja, Hamis Shengo aliisawazishia Lyon kwa mpira wa adhabu alioupiga na kwenda moja kwa moja wavuni na kumwacha Berko asijue la kufanya.
Kabla ya kufungwa bao hilo katika dakika ya 42, beki wa Yanga, Bakari Mbegu alimchezea vibaya kiungo Kassim nje kidogo ya eneo la 18, faulo ambayo ilitoa nafasi kwa vijana wa Lyon kupata sare 1-1 hadi mapumziko.Kipindi cha pili Yanga ilianza kwa kasi na katika dakika ya 47, Pius Kisambale alikosa bao kwa shuti lake kupanguliwa na kipa Juma Abdul na kutoka nje.
Kocha Sam Timbe aliwapumzisha Shamte, Kigi Makasi na Juma Seif na kuwaingiza Kenneth Asamoah, Rashid Gumbo na Godfrey Bonny mabadiliko ambayo yaliisaidia Yanga.
Mabadiliko hayo yaliisaidia Yanga kwa sababu Gumbo aliyechukua nafasi ya Kigi aliipatia Yanga bao la pili katika dakika ya 63 kwa shuti la umbali wa mita 32, lililomshinda kipa wa Lyon, Abdul.Washambuliaji wa Lyon, Adam Kingwande na Agustino Sino watajilaumu wenyewe kwa kupoteza nafasi nyingi za kufunga katika mechi hiyo.
Katika mechi hiyo pia Gumbo alipiga shuti kali ambalo liligonga mwamba katika dakika ya 71 na kutoka vile vile Kenneth Asamoah alishindwa kumalizia pasi Kisambale akiwa ndani ya 18. Katika mechi hiyo kocha wa Lyon alifanya mabadiliko mapema, ambapo katika dakika ya 16 alimtoa Benedictor Jacob na kumwingiza Sammy Kessy pia baadaye alimtoa Kessy na kumwigiza Jacob Masawe.
Licha ya kuwapo ulinzi mkali kwenye uwanja wa Azam, wapo baadhi ya mashabiki waliruka ukuta ambao sio mrefu sana na kuingia uwanjani.Yanga: Yaw Berko, Shadrack Nsajigwa, Abuu Zuberi, Bakari Mbegu, Chacha Marwa, Juma Seif, Shamte Ally, Nurdin Bakari, Davis Mwape, Pius Kisambale na Kigi Makasi.
African Lyon: Juma Abdul, Aziz Sibo, Hamis Shengo, Shaban Aboma, Hamis Yusuph, Razaki Khalfan, Adam Kingwande, Seleman Kassim, Benedictor Jacob, Hood Mayanja na Agustino Sino.
No comments:
Post a Comment