Maftah- Yanga walitaka kuua kipaji changu
BEKI wa kushoto wa timu ya taifa, Taifa
Stars na Klabu ya Simba, Amir Maftah ameamua kuweka wazi kile
kilichomtokea wakati akiwachezea watoto wa Jangwani, Yanga Afrika.
Katika mahojiano maalumu na safu hii, Maftah anasema kwamba ana
mshukuru Mungu kwa sasa yupo kwenye timu ambayo ina viongozi wanaotambua
mchango wake na wasio na mizengwe kama ilivyokuwa kwa upande wa Yanga.Anasema; “Kwa hakika kabisa naamini hivi sasa nisingekuwepo tena kwenye ulimwengu wa soka, kwani pale Yanga nilifanyiwa mambo ya ajabu mno yaliyokuwa yanatishia majaliwa yangu ya baadaye.”
Anasema licha ya kuichezea Yanga kwa moyo wake wote na mapenzi makubwa aliyokuwa nayo, lakini alishangaa kujikuta akihusishwa na kuihujumu timu hiyo.
“Kiukweli, mimi nilikuwa naipenda Yanga tangu nikiwa mdogo kabisa, malengo yangu yalikuwa ni kuhakikisha siku moja nakuja kuichezea.
“Mapenzi na Yanga yalikuwa ni ya kutoka moyoni kabisa, lakini niliyoyakuta, na mizengwe niliyofanyiwa, kwa hakika kabisa naweza kusema hakuna klabu ninayoichukia kama Yanga.
“Hata ninapocheza dhidi ya Yanga huwa nafurahi mno kuhakikisha tumewanyanyasa tunavyotaka na kuwafunga, kwani siipendi kabisa Yanga.
“Na katika kila mchezo nitahakikisha nacheza kufa au kupona kuhakikisha tu furaha nyangu ya kulipiza kisasi cha waliyonifanyia inatimia.”
Anasema wakati akiwa katika Klabu ya Mtibwa ya Manungu Turiani mkoani Morogoro, Simba walimfuata mara kadhaa kwa ajili ya kutaka kumsajili, lakini yeye akaikataa ofa hiyo.
“Niliikataa Simba kwa sababu tu nilikuwa na mapenzi makubwa na Yanga, hivyo sikutaka kuwachezea watoto hao wa Msimbazi, kwani akili yangu ilikuwa kwa watoto wa Jangwani.
“Na hata Yanga waliponifuata kwa ajili ya kutaka kunisajili sikuwa na kipingamizi, kwa sababu tayari walikuwa moyoni mwangu, hivyo nikatua kwao.” Maftah anasema licha ya kucheza kwa kujituma wakati akiwa na Yanga, lakini alishangaa kuona mizengwe ya hapa na pale kutoka kwa viongozi wa timu hiyo.
Anasema awali alichukulia ni mambo ya kawaida, lakini siku jinsi zilivyokuwa zinakwenda, akajiridhisha kwamba viongozi hao hawakuwa na nia nzuri na yeye.
“Ilifikia kipindi eti nikawa nashutumiwa kwamba mimi naihujumu Yanga kwa sababu ni mpenzi wa Simba, kitu ambacho kwangu kilikuwa kigeni kabisa kukisikia, lakini niliamua kuvumilia.
“Hata hivyo, kuna siku nitamuweka hadharani kiongozi mmoja wa Yanga ambaye alisababisha matatizo yote haya kiasi kwamba hadi mimi kuonekana msaliti.” Maftah anasema baada ya kuachwa na Yanga katika mazingira ya kutatanisha, alikuwa na wakati mgumu mno kwenye mustakabali wa maisha yake ya soka.
“Mimi ajira yangu ni soka. Soka ndiyo ninayoitegemea kuendesha maisha yangu ya kila siku pamoja na familia yangu, hivyo kuacha soka maana yake ni kwamba nakosa ajira. “Nilisota, huku nikijaribu kuangalia muelekeo utakuwaje, lakini namshukuru Mungu kwamba Simba wakaniona na wakanisajili kwa mkataba mnono.”
Anasema baada ya kutua Simba aliona mambo mengi ni tofauti, kwani viongozi wake walikuwa wanaonyesha kumjali kila mchezaji na hakuna mizengwe yoyote inamkera.
“Kwa uhakika kabisa naweza kusema hapa Simba nimefika, kwani viongozi wake wanawajali wachezaji na hata kiwango changu kimezidi kuimarika kwa sababu akili yangu yote ipo kwa ajili ya kuhakikisha inafanya vizuri katika kila mchezo.
“Simba wananilipa dola 600 kwa mwezi (sawa na zaidi ya shilingi 900,000) ambazo kwangu zinanitosha kabisa, hasa ukizingatia kwamba tunapata posho katika kila mechi, hivyo sina tatizo.”
Katika kuonesha shukrani zake, Maftah anasema kwamba amekuwa anajifua mno kivyake kuhakikisha kwamba anaendelea kuwa fiti ili kuweza kucheza katika kiwango cha juu kabisa.
Anasema hatarajii kuichezea timu nyingine kwa hapa Tanzania, kwani iwapo ataondoka Simba ndiyo utakuwa mwisho wake kama hatakuwa amepata timu nje ya nchi.
“Kwa kweli kwa upande wangu nikitoka hapa Simba, sina mpango wa kucheza katika timu yoyote ya hapa Tanzania, kwani kama sitapata timu ya nje ya nchi basi huo utakuwa ni mwisho wangu wa kucheza soka.”
Maisha kwenye Filamu Aidha Maftah anasema kwamba yupo kwenye hatua za mwisho za kukamilisha filamu yake inayozungumzia ukweli halisi wa soka la Tanzania (A True Story of Tanzanian Football).
Anasema kwenye filamu hiyo ataonesha matukio yote halisi ya mwenendo wa mchezo huo nchini pamoja na mwendendo wa klabu zinazoshiriki Ligi Kuu Tanzania Bara.
“Humo kutakuwa na kila kitu kinachohusu maisha ya soka la Tanzania pamoja na historia yangu nilikozaliwa na nilikoanza kucheza soka.
“Pia nitazungumzia kwa kina yale yote yaliyonitokea katika maisha yangu ya soka kwa uhalisia wote.”
Anasema katika filamu hiyo atamshirikisha gwiji wa soka la zamani hapa nchini Zamoyoni Mogella pamoja na wasanii wengine ambao hakuwa tayari kuwataja kwa sababu bado hajakamilisha nao mazungumzo.
“Kutakuwa na watu wengi kwenye filamu hii ambayo inatengenezwa na kampuni ya Asaa chini ya Meneja wangu, Imam Maunda.”
No comments:
Post a Comment