Oct 31, 2011

Yanga New Force



  • Kocha wa Yanga kosta Papic akishangilia ushindi pamoja na wachezaji wa timu hiyo.

  • OLIVER ALBERT
    KOCHA mpya wa Yanga, Kosta Papic, amedhihirisha kuwa ni fundi wa mechi za watani wa jadi, baada ya kuiongoza Yanga kuiliza Simba bao 1-0 katika mechi ya Ligi Kuu Tanzania Bara iliyochezwa jana Jumamosi Uwanja wa Taifa, jijini Dar es Salaam.

    Kwa matokeo hayo, Yanga imejiimarisha katika nafasi ya pili kwani imefikisha pointi 24 na kuwa pointi tatu nyuma ya Simba inayoendelea kushikilia usukani ikiwa na pointi 27.

    Karata ya Papic
    Kwa ushindi huo, Papic, ambaye ni raia wa Serbia, sasa ameifunga Simba mara nne katika mechi saba alizokutana nayo tangu alipokuja nchini mara ya kwanza Oktoba, 2009.

    Hakika viongozi wa Yanga walisoma alama za nyakati kwa kucheza kamari ya kumtimua Mganda, Sam Timbe, na kumkabidhi kazi Papic, ambaye alitua nchini Oktoba 27 na kuanza kazi rasmi Jumatatu iliyopita.

    Kumbuka Papic aliondoka nchini Februari mwaka huu na nafasi yake ilichukuliwa na Timbe, ambaye katika kipindi kifupi alichokuwa na Yanga, aliipa ubingwa wa Tanzania Bara na Kombe la Kagame.

    Hata hivyo, pamoja na mafanikio hayo na rekodi ya Timbe ya kutwaa Kombe la Kagame na timu nne tofauti za Atraco ya Rwanda, SC Villa na Polisi za Uganda, bado Yanga ilimrudisha Papic, ambaye ana uzoefu na mechi za watani wa jadi barani Afrika.

    Kwa ushindi huu, sasa Yanga itafurahia kulamba dume kwa kumchukua Papic, ambaye ana sifa ya kuwa kati ya makocha wachache kuaminiwa kuzinoa timu zenye upinzani za Afrika Kusini za Kaizer Chiefs na Orlando Pirates.

    Pia timu nyingine alizozinoa ni Hearts of Oak ya Ghana yenye upinzani mkali na Asante Kotoko ya huko. Bila kusahau Nigeria alikoinoa Enugu Rangers, ambayo ina uhasama na Ibadan Shooting Stars.

    Pia aliwahi kuzifundisha Enyimba na Lobi Stars za Nigeria bila kusahau Martzburg ya Afrika Kusini.

    Kicheko cha viongozi wa Yanga kitaongezeka zaidi kwani Papic ndiye alimsajili, Davies Mwape, ambaye alifunga bao pekee la timu hiyo jana Jumamosi.

    Bao la Mwape
    Kabla ya pambano hilo lililoanza kwa timu hizo kuogopana, kulikuwa na imani kuwa Papic atarejesha morali Yanga baada ya kuwa chini katika siku za karibuni.

    Mwape ni kati ya wachezaji waliokuwa wanatakiwa kuinuliwa kiwango kutokana na siku za karibuni kuumia misuli.

    Mzambia huyo ambaye alisajiliwa kutoka Konkola United Novemba mwaka jana, kutokana na kuwa majeruhi alilazimika kukaa nje mechi tatu zilizopita dhidi ya Toto African, JKT Oljoro na Kagera Sugar.

    Ujio wa Papic unaelekea umemsaidia Mwape, ambaye alikuwa mwiba kwa mabeki wa Simba walioongozwa na Victor Costa �Nyumba�.

    Mabeki wa Simba walikumbana na kibarua kigumu baada ya Papic kuchezesha washambuliaji watatu; Mwape, Hamisi Kiiza na Kenneth Asamoah, ambaye pia aliletwa kikosini na Papic.

    Kitendo hicho kiliwavuruga mabeki wa Simba, ambao walizoea kuona Yanga ikicheza na washambuliaji wawili wakati ikiwa chini ya Timbe.

    Kuchanganyikwa kwa mabeki wa Simba na mfumo wa Papic ambao ulisababisha kashikashi nyingi zilizoongozwa na Asamoah, ambaye alikosa nafasi nyingi, ni wazi ziliisaidia Yanga kupata bao lake.

    Mwape alifunga bao hilo la ushindi dakika ya 72 kwa shuti la karibu, baada ya kuuwahi mpira uliowababatiza mabeki wa Simba, Costa na Juma Nyosso, ambao walishindwa kumiliki mpira mrefu uliopigwa na kipa wa Yanga, Yaw Berko.

    Baada ya bao hilo, wachezaji wote wa Yanga walimkimbilia kocha Papic, wakamrukia na kumkumbatia kwa furaha kubwa, katika tukio lilivuta hisia nyingi.

    Inawezekana walifanya hivyo kama ishara ya kumkaribisha
    Simba itabidi ijilaumu yenyewe
    Kocha wa Simba, Moses Basena, ambaye alikuwa anakabiliana na Yanga kwa mara ya tatu mwaka huu, baada ya kuifunga mara moja na kufungwa mara moja, bila shaka atakuwa amewasomea risala kali washambuliaji wake waliopoteza nafasi nyingi za wazi.

    Simba, ambayo imepoteza mchezo wake wa kwanza, iliingia katika mchezo huo ikijivunia washambuliaji hatari Mganda Emmanuel Okwi na Mzambia Felix Sunzu, lakini hawakufua dafu mbele ya ukuta wa Yanga ulioongozwa na Nadir Haroub �Cannavaro�, ambaye aling�ara katika mchezo huo.

    Ukuta wa Yanga ulichangamka zaidi katika kipindi cha pili, ingawa hakukuwa na maelewano mazuri kati ya Cannavaro na Chacha Marwa.

    Hata hivyo, washambuliaji wa Simba mara nyingi walipofika kwenye eneo la hatari walishikwa na kigugumizi na kwa kiasi kikubwa kuigharimu timu yao.

    Simba iliuanza mchezo huo kwa kasi na Okwi alipiga shuti kali lililotoka nje katika dakika ya pili.

    Dakika moja baadaye, beki wa Yanga, Chacha Marwa, nusura ajifunge wakati akiokoa shuti jingine la Okwi.
    Sunzu alikosa kasi na akawa anapoteza mipira mingi kwenye safu ya ushambuliaji.

    Kwa mfano alipata nafasi nzuri dakika ya 41 baada ya kupokea pasi nzuri ya Okwi, lakini badala ya kufunga, alianza mbwembwe za kutuliza na kugeuka na mabeki wa Yanga wakawahi kuondosha hatari wakati yeye akianguka chini.

    Katika dakika ya 50, mpira wa kichwa wa Sunzu ulikwenda nje baada ya kuunganisha krosi ya beki wake wa kushoto, Juma Jabu.

    Simba ikiongozwa na Patrick Mafisango, ilimzonga mwamuzi, Oden Mbaga, katika dakika ya 60 kudai penalti baada ya Godfrey Taita, kumwangusha Okwi eneo la hatari. Mwamuzi alitoa adhabu ndogo, ambayo waliipoteza.

    Okwi alipoteza nafasi mbili nzuri katika dakika za 81 na 87 baada ya kupiga mashuti yake nje.

    Kosa kosa za Yanga
    Katika dakika ya tisa, Kiiza, alikosa nafasi ya wazi akiwa na kipa Juma Kaseja kufuatia krosi safi ya Oscar Joshua.
    Mwape naye alikosa nafasi ya wazi baada ya kupiga shuti lililookolewa na kipa Kaseja baada ya kuwatoka mabeki wote wa Simba katika dakika ya 11.

    Dakika moja baadaye, Asamoah, alikosa nafasi ya wazi baada ya kuwapiga chenga Nyosso na Costa, lakini akapiga shuti lililokwenda fyongo.

    Katika dakika ya 14, Amri Kiemba, alishindwa kujaza mpira wavuni baada ya kupewa pande kali na Okwi.
    Asamoah alipoteza nafasi nyingine dakika ya 27 baada ya kupiga shuti lililopaa.

    Tegete naye alikosa nafasi nzuri ya wazi katika dakika ya 90, baada ya shuti lake kutoka nje na kugonga nyavu ndogo.

    Maoni ya makocha
    Akizungumza baada ya mchezo, Papic, alikuwa mkweli kwa kueleza ushindi wa timu yake ulichangiwa na bahati zaidi, akikiri hakukuwa na ufundi wowote katika ushindi huo.

    Alisema alikuwa na timu kwa siku tatu tu na kuongeza kuwa walichofanya wachezaji wake, ni kutumia vizuri makosa ya mabeki wa Simba.

    Alisema kuna kazi kubwa mbele ya kuhakikisha timu hiyo inaendelea kushinda ili kuipiku Simba kileleni.

    Naye Basena alilia na wachezaji wake kushindwa kutumia nafasi walizopata, akiwataja zaidi Okwi na Amri Kiemba.
    Alisema pia beki yake ilicheza kwa kiwango cha chini na hasa Costa, ambaye makosa yake yalitoa mwanya kwa Mwape kufunga.

    Timu
    Yanga: Yaw Berko, Godfrey Taita, Oscar Joshua, Chacha Marwa, Nadir Haroub �Cannavaro�, Juma Seif, Nurdin Bakari, Haruna Niyonzima, Kenneth Asamoah, (Rashid Gumbo dk. 89), Davies Mwape (Jerry Tegete dk. 76) na Hamisi Kiiza (Idrissa Rashid dk. 54).

    Simba: Juma Kaseja, Nassor Said �Cholo� (Mafisango dk. 25), Juma Jabu, Juma Nyosso, Victor Costa, Jerry Santo, Shomari Kapombe, Amri Kiemba (Haruna Moshi �Boban� dk. 45), Felix Sunzu, Emmanuel Okwi na Ulimboka Mwakingwe (Moshi Kazimoto dk.68).

No comments: