Oct 20, 2011

Simba 'full' shangwe Yanga yaiva Toto leo



Mshambuliaji wa Simba, Ulimboka Mwakingwe (kushoto) akimtoka beki wa Ruvu Shooting, George Michael (kulia) katika mechi ya Ligi Kuu Tanzania Bara iliyochezwa jana kwenye Uwanja wa Chamazi jijini Dar es Salaam. Simba ilishinda 2-0. Picha na Jackson Odoyo
 Calvin Kiwia na Jesca   NangawMABINGWA wa Ngao ya    Jamii, Simba jana waliendelea kujiimarisha kileleni mwa Ligi Kuu kwa kuichakaza Ruvu Shooting mabao 2-0 kwenye Uwanja wa Chamazi jijini Dar es Salaam, huku watani zao Yanga wakishuka dimbani leo kuikabili Toto African.

Vinara hao walilazimika kusubili hadi kipindi cha pili kusherekea pointi tatu muhimu kwa vijana hao Msimbazi shukrani kwa mabao ya Emmanuel Okwi na Haruna Moshi aliyeingia akitokea benchi na kuifanya Simba kufikisha pointi 24.

Katika mechi hiyo iliyopigwa kwenye uwanja wa Azam, Chamazi, nje kidogo ya jiji na kuhudhuriwa na watazamaji wachache kulinganisha na mechi zingine za Simba kwenye uwanja huo, ilikuwa na upinzani mkali tangu mwanzo mpaka mwisho.

Kiu ya kutaka kufunga mabao kwa Simba ilianza kwa shambulizi la dakika ya kwanza ya mchezo, baada ya washambuliaji wake Okwi, Felix Sunzu na Uhuru Seleman kugongea vizuri kabla ya jitihada zao kutibuliwa na mabeki wa Ruvu Shooting.

Ruvu Shooting inayoundwa na wachezaji chipukizi, ilijibu shambulizi hilo dakika saba baadaye, lakini kiki ya Abdallah Juma ilipaa juu ya lango, huku Jerry Santo wa Simba naye akikosa kwa staili hiyo ya kupaisha mpira juu ya mwamba dakika ya 18.

Vinara hao wa Ligi Kuu walitawala sehemu kubwa ya kipindi cha kwanza, na nusura wabadilishe matokeo kama shuti la Uhuru  lisingegonga mwamba na kurudi uwanjani kufuatia gonga nzuri na Sunzu.

Mabadiliko yaliyofanywa na kocha wa Simba, Moses Basena ya kumtoa Uhuru na kumuingiza kiungo Haruna Moshi 'Boban' dakika ya 46, yalizaa matunda dakika moja baadaye kufuatia kazi nzuri ya Boban kumwezesha Okwi kufunga bao la kuongoza kirahisi kutokana na mabeki wa Ruvu kujichanganya.

Washambuliaji Simba waliojenga 'netiweki' nzuri ya ushambuliaji langoni mwa Ruvu baada ya kupewa 'dawa' ya kuongeza hamu ya kufunga mabao kama alivyodai kocha Basena, waliandika bao la pili safari hii likiwekwa kimiani na Boban.

Kocha wa Basena alisema wachezaji wake walicheza vizuri na kutegeneza nafasi nyingi za kufunga ni jambo la kujivunia kwa sababu uelewana wao umetoa ushindi.

Boban aliyeonekana kucheza vizuri na Okwi alifunga bao hilo kwa shuti kali dakika ya 54 na kumwacha kipa wa Ruvu, Benjamin Haule aliruka bila mafanikio.

Kocha wa Ruvu, Boniface Mkwasa alifanya madadiliko ya kuwatoa Abdallah Juma na  Raphael Keyala na nafasi zao kuchukuliwa na Seif Abdallah na Abdallah Abraham.

Mabadiliko hayo yaliwapa nguvu Ruvu baada ya kufanya mashambulizi matano langoni mwa Simba katika muda mfupi, lakini yaliishia mikononi kwa kipa Juma Kaseja au kutibuliwa na mabeki wa Simba.

Ushindi huo umeifanya Simba kuzidi kujiimarisha kileleni mwa msimamo kwa kufikisha 24, baada ya michezo 10, huku ikiendeleza rekodi yake ya kutopoteza mchezo mpaka sasa.

Mkwasa amesikitika kwa washambuliaji wake kutegeneza nafasi nyingi na kushindwa kuzitumia anajipanga kwa wakati ujao.
Wakati huo huo, ligi hiyo inaendelea tena leo kwa mabingwa watetezi Yanga kuwavaa ndugu zao wa Toto African kwenye Uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam.

Yanga wanaingia kwenye mchezo huo wakiwa na kumbukumbu nzuri dhidi ya Toto mara ya mwisho walipokutana msimu uliopita mabingwa hao walishinda kwa mabao matatu.

Makocha wa pande zote mbili wameapa kuweka undugu pembeni na kuhaidi mchezo kusaka pointi tatu muhimu kwa kila mmoja.

Akizungumza wakati wa mazoezi ya jana asubuhi kocha mkuu wa Yanga, Sam Timbe amesema anafahamu ubora na kiwango cha wapinzani wao na kikosi chake kipo kamili kukabiliana na wapinzani wao.

"Kila mmoja wetu anataka ushindi, nategemea upinzani mkubwa kwani timu ya Toto Afrikan ni nzuri na kila tukikutana nayo kunakuwa na upinzani mkubwa, wachezaji wote wako kwa sasa wako kwenye hali,"alisema Timbe.

Naye kocha wa Toto, John Tegete amesema historia si kigezo cha wao kupoteza kwani msimu huu wamejidhatiti kikamilifu kufuta uteja.
Tegete alisema kikosi chake kiko imara kukabiliana na mabingwa hao na anategemea mchezo kuwa mgumu kutokana na kila mmoja wao kuhitaji ushindi kwa namna yoyote.

Alisema wamecheza na Yanga mara nyingi na anatambua upinzani unaokuwepo mara timu hizo zinapokutana hivyo hana wasiwasi wowote kukabiliana na kikosi hicho huku akitamba wapo kamili kuivaa Yanga.

"Sitegemei mteremko wowote licha ya timu hizi kuwa karibu na sisi tupo ugenini kwa sababu huu ni ushindani na kila mmoja anataka apate nafasi ya kuwa katika nafasi nzuri kwenye msimamo," alisema Tegete kwa akijiamini.

Yanga yenye pointi 15 ikiwa nafasi ya nne katika msimamo inashuka uwanjani ikiwa na kumbukumbu ya ushindi kiduchu dhidi ya Kagera Sugar katika mchezo uliopita huku wapinzani wao Toto wakiwa na pointi10 na kukamata nafasi ya tisa.
chanzo na   www.mwananchi.co.tz

No comments: