Oct 18, 2011

Mwasika, Nsajigwa warejea


NI habari mbaya ambazo Simba hawatapenda kuzisikia za mabeki wa pembeni wa Yanga, Shadrack Nsajigwa na Stephano Mwasika kurejea uwanjani na kuanza mazoezi jana Jumatatu.

Mwanaspoti iliwashuhudia mabeki hao wenye sifa ya kuzuia na kupandisha mashambulizi wakijifua na wenzao kwenye mazoezi makali yaliyokuwa yakisimamiwa na kocha Sam Timbe kwenye Uwanja wa Kaunda jijini Dar es Salaam.

Daktari wa Yanga, Dk. Juma Sufiani alidokeza kuwa wakali hao, ambao pia ni tegemeo la Taifa Stars watakuwa fiti kuivaa Simba, Oktoba 29.

Sufiani alisema mabeki hao wanahitaji mazoezi ya wiki moja tu na watakuwa fiti kucheza mechi yoyote kuanzia Oktoba 24, mwaka huu.

Yanga na Simba zitakutana kwenye pambano la Ligi Kuu Bara Oktoba 29 jijini Dar es Salaam ikiwa ni mara ya tatu tangu mwaka huu kuanza baada ya kuvaana kwenye Kombe la Kagame Julai 10 na katika Ngao ya Hisani, Agosti 17, mwaka huu.

Mwasika alifanyiwa upasuaji wa goti nchini India mwezi Juni, mwaka huu, baada ya kuumia kwenye mazoezi ya Taifa Stars.

Nsajigwa, ambaye ni nahodha wa Yanga na Stars, naye aliumia nyonga kwenye mazoezi ya Stars ilipokuwa inajiandaa na pambano la kusaka tiketi ya kucheza fainali za Kombe la Mataifa ya Afrika dhidi ya Morocco.

Mwasika alirejea kwa kishindo na kutishia amani ya beki mwenzake Oscar Joshua baada ya kufunga bao kwa shuti kali lililomshinda kipa Shaaban Kado na kujaa kimiani kwenye mazoezi ya timu hiyo.

Katika hatua nyingine, kocha wa timu hiyo, Sam Timbe amedai hakuna tatizo kwa Mwasika kurejea uwanjani kwani ataendelea kupanga kikosi kwa kulingana na uwezo mchezaji aliouonyesha kwenye mazoezi.

"Siwezi kumuonea aibu mchezaji yeyote yule kumweka benchi kama atashindwa kuonyesha bidii na kujituma kwenye mazoezi yangu," alisisitiza Timbe, ambaye anashikilia rekodi ya kutwaa Kombe la Kagame na timu tatu tofauti na Yanga, Atraco ya Rwanda, SC Villa na Polisi za Uganda.

No comments: