Oct 24, 2011

YANGA WAOMBA ARDHI KWA SERIKALI - KUJENGA UWANJA MPYA WA KISASA



Uongozi wa mabingwa soka Tanzania Bara, Yanga ya jijini Dar es Salaam, umeiandikia barua Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi kuomba kiwanja ambacho wanatarajia kujenga uwanja wa kisasa hivi karibuni.
Akizungumza jijini Dar es Salaam jana, Katibu Mtendaji wa klabu hiyo, Celestine Mwesiga, alisema, wameiandikia barua wizara hiyo, kutaka kupewa kiwanja cha hekari 20 katika Manispaa ya Kinondoni au Ilala, ili waweze kutimiza ndoto yao ya kutaka kumiliki kiwanja hicho cha kisasa kama ilivyo kwa klabu mbalimbali duniani.
“Tumeishafanya mawasiliano na wenzetu wa Wizara ya Ardhi kuomba kupatiwa kiwanja hicho na wameonyesha wapo tayari kutufanikishia lengo letu, hivyo tunasubiri wakati wowote watujulishe wapi wametupata,” alisema Mwesiga.
Alisema uongozi wake umejipanga kuhakikisha unajenga uwanja huo, ili Yanga iweze kupunguza gharama mbalimbali zinazolipwa kupitia viwanja wanavyochezea sasa, ili waweze kujiimarisha kiuchumi.
Akifafanua kuhusu uwanja huo, Mwesiga alisema utakuwa na bwawa la kuogelea, uwanja wa tenisi, mpira wa mikono, sambamba na hosteli kwa ajili ya wachezaji wa klabu hiyo.
Hivi karibuni, watani zao Simba walitangaza mikakati mbalimbali kujenga vitega uchumi ikiwamo kujenga jengo la ghorofa 12 yalipo makao makuu ya klabu hiyo mtaa wa Msimbazi sambamba na uwanja wa kisasa ‘Simba Sports Arena, huko Bunju nje kidogo ya jiji.
chanzo na 
http://www.shaffihdauda.com

No comments: