Nov 21, 2011

Yanga inatia raha


                                           kikosi cha yanga                                                                                                      
                                                                                                              
                                                                                                  MICHAEL MOMBUR


KAMA wewe ni shabiki wa Yanga, shusha pumzi kwanza. Ukisikia maneno wanayozungumza matajiri wanaofanya usajili unaweza kuchanganyikiwa kwa furaha. 

Viongozi hao wamepania kufanya usajili wa bandika bandua na tayari wameanza kumnyemelea beki matata wa kati kutoka Zanzibar ambaye akitua tu Jangwani, shughuli imekwisha.

Makamu Mwenyekiti wa Kamati ya Usajili ya Yanga, Seif Ahmed Seif Magari, aliiambia Mwanaspoti jana Ijumaa kwamba mambo yanakwenda kisayansi na timu itakuwa imara mno katika mzunguko wa pili wa Ligi Kuu Tanzania Bara.

Kiongozi huyo alisema kwamba: Kuna beki wa kati mahiri sana kutoka Zanzibar, tunaendelea kumfuatilia na nadhani ndani ya wiki moja tutakuwa tumejua kama tutamsainisha au la, lakini rekodi zake zinaonyesha ni beki kiboko.

Kocha anaendelea kumfuatilia kwa karibu sana na hakuna chochote kilichofanyika rasmi mpaka sasa, ndiyo maana siwezi kutaja jina lake wala klabu anayotoka.

Aliongeza: Athuman Idd tumemrudisha na kocha amekubaliana naye na kwamba ataendelea kumwangalia kwa muda fulani, Salum Telela na Omega Seme waliokuwa Moro United kwa mkopo pia wamerudi kikosini.

Unaweza kuona kwamba Yanga katikati kuna mashine kali Haruna Niyonzima, Nurdin Bakari, Godfrey Bonny, Rashid Gumbo, Seif Juma �Kijiko, Omega na Chuji mwenyewe.

Ni wachezaji ambao wanaweza kufanya chochote muda wowote.
Bonny alikuwa hatumiki sana, lakini ni mzoefu, Gumbo ni kiungo, lakini anahamishiwa mara nyingi kwenye winga, angalia Nurdin anacheza popote beki, kiungo, mshambuliaji yaani anapachikwa tu kuendana na matakwa na malengo ya kocha.

Mwone Haruna, anaweza kucheza namba 10 pia, yaani Yanga hii tuliyosajili itakuwa inatumia viungo wengi sana kwa wakati mmoja kwa mujibu wa kocha, na siyo ajabu siku moja ukaona wakicheza hata watano kwa mpigo, tumejiwekea malengo ya mbali sana na tunataka kubadili kabisa staili ya mchezo.

Tunalenga mzunguko wa pili na mashindano ya kimataifa. Ubingwa tunautaka lakini akili nyingi tumeziweka kwenye Ligi ya Mabingwa Afrika mwakani, tunataka kufanya kitu cha tofauti kabisa.
MWISHO. chanzo na mwanaspoti

No comments: