Nov 22, 2011

Ndolanga afunguka soka ya vijana

 



Mshambuliaji wa timu ya vijana ya Simba, Miraji Athumani (kushoto),akiwania mpira na beki wa JKT Oljoro kwenye mechi ya robo fainali ya Michuano ya Vijana ya U-20 inayoendelea kwenye Uwanja wa Karume jijini Dar es Salaam. Simba ilishinda mabao 6-2. Picha na Michael Matemanga.
Mwandishi Wetu


MWENYEKITI wa zamani wa Chama cha Soka Tanzania, FAT, (sasa Shirikisho la Soka Tanzania-TFF), Muhidin Hamad Ndolanga amesema hajaona uwapo wa nia ya dhati ya shirikisho hilo kuwekeza na kuendeleza soka ya vijana ikilinganisha kipindi chake.

Akizungumza katika mahojiano maalum jana Makao Makuu ya TFF, Ndolanga alisema: "Nilipokuwa naondoka FAT, niliacha misingi ya soka ya vijana, lakini kwa sasa sioni kama kuna seriousness (umakini zaidi) katika kuendeleza soka ya vijana.

Ndolanga, alisema kwa sasa kuna mashindano mbalimbali ya vijana yanaendeshwa lakini baada ya hapo yanaishia njia na hivyo kutokuwa na faida kwa vijana."Nadhani cha kufanya hapa, inatakiwa kuanza kutengeneza watoto tangu wakiwa darasa la nne na hadi kumaliza kidato cha sita, watapatikana timu za miaka mbalimbali.

"Wakiwa kidato cha nne, watakuwa wana sifa za kucheza U-17 kwa kuwa watakuwa na miaka 17 na akiwa kidato cha sita watakuwa na miaka 19 hivyo wanaweza kucheza U-20, utaratibu huu unawezekana.

"Hivi sasa kuna wadhamini wengi, wanaweza kuwaanzishia mashindano kila umri, angalia hapa, kuna mashindano ya vijana ya U-20 yanayodhaminiwa na Uhai, sasa kuna watu wana hela zao, ni mipango tu na taratibu zikiwekwa.
Ndolanga aliyeshindwa na Tenga kwenye uchaguzi wa kwanza wa TFF, 2004 alisema kuwa TFF ikiwekeza katika madarasa hayo, kwanza itakuwa na timu nyingi kwa umri mbalimbali na pia vijana ni rahisi kuwajenga kitabia kuliko waliokomaa.

Ndolanga ambaye wakati wa uongozi wake FAT, wadau walishuhudia mizozo ya uongozi ya mara kwa mara na aliyekuwa katibu mkuu wake, Michael Wambura alisema ili nchi ifikie mafanikio katika soka, uwekezaji katika eneo hilo ni jambo lisilokwepeka.

"Mtoto anajengeka kitabia, unamfundisha anaelewa nini maana ya soka na nini haramu ya soka, lakini si wazee (wachezaji wakongwe)," alisema Ndolanga.

Alisema kuwa TFF isiogope gharama kutengeneza wachezaji kwani kama itawekeza na wakapatikana wachezaji wazuri, inaweza kufanya utaratibu wakauzwa nje na yenyewe kupata fedha."Wenzetu wanafanya hivyo, wanatumia pesa nyingi kuwekeza kwenye soka la vijana na baadaye wanavuna faida kubwa."

"Watafutwe wadhamini kwa ajili ya kuendeleza vijana, na waendelezwe pindi wanapopatikana na si kuwaacha wanapotea hewani," alisema Ndolanga aliyesisitiza kuwa kuna wadhamini wengi wanaopenda kudhamini soka mradi kuwepo na utaratibu kwa udhamini.
 chanzo na mwanannchi

No comments: