Nov 1, 2011

Simba wasaka faraja, Yanga vitani

OLIVER ALBERT
BAADA kulizwa na watani wao, Simba watasaka faraja kutoka kwa Moro United wakati Yanga itakuwa katika vita dhidi ya Polisi wakati timu hizo zitakapokabiliana kwenye Uwanja wa Jamhuri mjini Dodoma wakati wa mechi za kufunga mzunguko wa kwanza wa Ligi Kuu Tanzania Bara zitakazochezwa kesho Jumatano.

Simba inayoongoza Ligi Kuu ikiwa na pointi 24 baada ya kufungwa na wapinzani wao wa jadi, Yanga 1-0 itapenda kutuliza mzuka wa mashabiki wake kwa kuifunga Moro United kwenye Uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam ili kuhakikisha inabaki kwenye usukani wa Ligi Kuu.

Yanga kwa upande wake, itakuwa inaiombea mabaya Simba wakati huo ikipigana kuifunga Polisi ili kuwakamata wapinzani wao wa jadi. Yanga ipo pointi tatu nyuma ya Simba.
Sala za Yanga zinaweza kufanikiwa ikiwa Simba wataendeleza harakati za kumsaka mchawi baada ya kufungwa na watani zao. Ni kawaida kwa klabu hizi kubwa mbili kuingia katika migogoro pale zinapofungwa na mtani wake.
Sasa kuna maneno tayari kuwa ajira ya kocha wa Simba, Moses Basena ipo hatarini baada ya kufungwa na Yanga.

Simba wameshasahau kuwa Mganda huyo amesaidia timu hiyo kuongoza ligi na kabla ya kukabiliana na Yanga, ilikuwa haijapoteza mechi.

"Tusahau kipigo cha Yanga tuangalie mechi nyingine. Ule ni mchezo kama michezo mingine yoyote hivyo watu wasitishike kwa kupoteza, tunahitaji kushinda mchezo ujao dhidi ya Moro United ili tuweze kumaliza mzunguko wa kwanza tukiwa tunaongoza ligi.

"Ninachowaomba wachezaji wangu hasa washambuliaji kuwa makini, kwani tunaongoza kwa kutengeneza nafasi nyingi za kufunga kwenye ligi lakini hatuzitumii kutokana na papara ya washambuliaji wangu. Wanatakiwa kutulia ili timu iweze kupta mabao," alisema Basena, raia wa Uganda wakati alipozungumza na Mwanaspoti.

Naye kocha wa Moro United, Hassan Banyai alisema watahakikisha wanashinda mchezo huo na kuisimamisha Simba.

Kwa upande wao, Yanga wana nafasi kubwa ya kuvuna pointi tatu dhidi ya Polisi, ambayo inasuasua kwenye ligi hiyo. Polisi inashika nafasi ya pili kutoka mkiani ikiwa na pointi tisa.

Hata hivyo, wanapaswa kuchukua tahadhari ya uwanja wa Jamhuri, ambao unashutumiwa kuwa kati ya viwanja vibovu vya Ligi Kuu Tanzania Bara.

Kocha wa Yanga, Kostadian Papic, hata hivyo, amepania kuendeleza ubabe kwa kutamba kumnyoa kila ajaye mbele yake hadi wahakikishe wanaikamata Simba na kutwaa ubingwa wa Tanzania Bara.

Mechi nyingine zitakaochezwa kesho Jumatano zitakuwa kati ya JKT Oljoro itakaowakaribisha Villa Squad kwenye Uwanja wa Sheikh Amri Abeid jijini Arusha, Toto African watakuwa wenyeji wa Azam kwenye uwanja wa CCM Kirumba jijini Mwanza, JKT Ruvu watakuwa wageni wa ndugu zao Ruvu Shooting kwenye Uwanja wa Mlandizi mkoani Pwani na Mtibwa itaikaribisha African Lyon kwenye Uwanja wa Manungu. Kagera Sugar watakuwa wenyeji wa Coastal Union keshokutwa Alhamisi kwenye Uwanja wa Kaitaba mjini Bukoba. CHANZO NA http://www.mwanaspoti.co.tz

No comments: