Nov 5, 2011

Yondani ruksa Jangwani,Simba yanasa bonge la beki



MICHAEL MOMBURI
SIMBA iko tayari kufanya mazungumzo na Yanga ili iwauzie, Kelvin Yondani, muda wowote huku beki wa shughuli, Derrick Walulya, wa Uganda akiwa na nafasi kubwa ya kurejea Msimbazi, uongozi umethibitisha.

Wekundu wa Msimbazi hao pia wamemwachia kwa shingo upande kiungo Mkenya, Jerry Santo, anayekwenda Vietnam. Santo amekataa ofa ya kubaki Simba kwenye mzunguko wa pili wa Ligi Kuu Tanzania Bara.

Santo aliyekuwa akivaa jezi namba 13 amekuwa tegemeo kwenye kikosi cha kwanza cha Simba kwa misimu miwili mfululizo.

Makamu Mwenyekiti wa Simba, Geoffrey Nyange �Kaburu� aliiambia Mwanaspoti jana Ijumaa kuwa Santo hataichezea Simba mzunguko wa pili lakini Walulya, ambaye aliicheza timu hiyo kwenye Kombe la Kagame ana nafasi kubwa ya kurejea Msimbazi.

�Santo amemaliza mkataba na Simba na ametuaga kwamba anaondoka hawezi kurudi, tumembembeleza lakini amekataa ofa yetu mpya,� Kaburu alisema.

�Alisema anakwenda Vietnam tumemtakia kila la kheri, lakini tumemwambia kwamba mambo yakibadilika arudi muda wowote tutampokea.

�Ni mchezaji mahiri, tulipenda kuendelea naye lakini inaonekana akili yake ameigeuzia kwenye soka la nje zaidi.�
Kuhusu Yondani, ambaye amekuwa akihusishwa na Yanga, Kaburu alisema: �Yondani bado ni mchezaji wa Simba na tuna mkataba naye kisheria mpaka mwakani.

�Hatujapata ofa yoyote kwa klabu inayomhitaji, lakini timu yoyote hata kama ni Yanga ikija kwetu wakitupa ofa nzuri tutamwachia kama mchezaji mwingine yoyote yule, ili mradi tuelewane na dau lifikiwe.�

Lakini viongozi wazito kwenye Kamati ya Usajili ya Yanga, jana Ijumaa walisema kuwa hawako tayari kumnunua Yondani kwa dau kubwa labda kama atakubaliana na Simba wavunje mkataba kwa masharti mepesi.

Yondani amegoma kuchezea Simba katika siku za karibuni ikidaiwa kuchukizwa na kutopangwa katika kikosi cha kwanza cha timu hiyo.chanzo na http://www.mwanaspoti.co.tz

No comments: