ELECTIONS COMMITTEE
TAARIFA KWA VYOMBO YA HABARI
06 MACHI 2012
UFAFANUZI KUHUSU MAJUKUMU, WAJIBU NA MAMLAKA YA KAMATI YA UCHAGUZI NA
MAELEZO YA KINA KUHUSU MAAMUZI YA KAMATI ZA UCHAGUZI ZA TFF KUHUSU MAOMBI
YA NDG. MICHAEL RICHARD WAMBURA KUGOMBEA UONGOZI KWENYE UCHAGUZI WA
TFF 2008, UCHAGUZI WA KLABU YA SIMBA 2010 NA FAM 2011.
1. USIMAMIZI WA CHAGUZI ZA WANACHAMA WA TFF
Muundo wa Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) umeelezwa wazi kwenye Katiba ya TFF Ibara ya 18. Kamati ya Uchaguzi ya TFF ni moja kati ya vyombo sita vilivyoainishwa
katika Muundo wa TFF. Majukumu, wajibu na mamlaka ya vyombo vya TFF
yameainishwa katika Katiba ya TFF na Kanuni zilizotungwa na kuidhinishwa
na Kamati ya Utendaji ya TFF kwa kuzingatia Ibara ya 34 ya Katiba hiyo.
Majukumu,
wajibu na mamlaka ya Kamati ya Uchaguzi ya TFF yameainishwa kwenye
Katiba ya TFF Ibara ya 49 na kwenye Kanuni za Uchaguzi za TFF na Kanuni
za Uchaguzi za wanachama wa TFF. Mbali na majukumu na wajibu wa
kusimamia uchaguzi wa TFF na chaguzi za wanachama wake na kuishauri
Kamati ya Utendaji ya TFF kuhusu Kanuni za Uchaguzi, Kamati ya Uchaguzi
ya TFF inao wajibu wa kulinda Katiba na Kanuni za uchaguzi za TFF na
Katiba ya FIFA na Katiba za wanachama wa TFF kama ilivyotamkwa kwenye
Kanuni za Uchaguzi za TFF Ibara ya 6 na Kanuni za Uchaguzi za wanachama
wa TFF Ibara ya 26.
Uchaguzi Mkuu wa TFF hufanyika kwa mujibu wa Kanuni za Uchaguzi wa TFF.
Chaguzi za wanachama wa TFF na wanachama wao hufanyika kwa mujibu wa
Kanuni za uchaguzi za wanachama wa TFF na si vinginevyo. Kanuni hizi
zimeainisha taratibu mbalimbali ambazo lazima zizingatiwe kikamilifu,
ikiwa ni pamoja na utaratibu wa ukataji rufaa katika ngazi mbalimbali za
uchaguzi. Vyombo na Kamati zote za TFF,
Wanachama wote wa TFF na wanachama wao, na wadau wote wa soka wanao
wajibu wa kuheshimu Kanuni mbali mbali za TFF ambazo ni pamoja na Kanuni
za Uchaguzi.
2. MAAMUZI KUHUSU MAOMBI YA UONGOZI YA NDG. MICHAEL WAMBURA
Kwa
muda mrefu pamekuwepo na taarifa mbalimbali kupitia vyombo vya habari
zenye lengo la kuwafanya wadau na wapenzi wa soka na umma wa watanzania
kwa ujumla kuaminishwa kuwa Ndg. Michael Wambura huonewa na vyombo vya
TFF vinavyosimamia uchaguzi kila anapoomba nafasi za uongozi katika TFF.
Baadhi ya vyombo vya habari na baadhi ya wapenzi wa soka wamesikika
wakisema kwamba kuenguliwa kwa Ndg. Michael Wambura kugombea uomgozi ni
kutokana na kuogopwa na viongozi wa TFF. Kamati ya Uchaguzi ya TFF
inapenda kufafanua kwa kina maamuzi yote yaliyofanyika kuhusu maombi
yote ya uongozi ya Ndg. Michael Wambura na kuweka wazi vielelezo
vilivyotumika kufikia maamuzi hayo ili umma wa watanzania wafahamu
kinagaubaga ukweli kuhusu maamuzi hayo:
UCHAGUZI MKUU WA TFF 2008
Kamati
ya Uchaguzi ya TFF ilimwengua Ndg. Michael Wambura kugombea nafasi ya
Makamu wa kwanza wa Rais wa TFF kwa kutokidhi matakwa ya uadilifu kwa
mujibu wa Kanuni za Uchaguzi na Katiba ya TFF. Ndg. Michael Wambura
hakuridhika na uamuzi huo na alikata rufaa kwenye Kamati ya Rufaa ya
TFF. Hata hivyo baada ya Kamati ya Rufaa kupitia nyaraka mbali mbali
zilizowasilishwa kwenye Kamati hiyo ikiwa ni pamoja na ripoti ya ukaguzi
wa maheabu ya TFF/FAT kwa mwaka 2002, 2003 na 2004 rufaa yake
ilishindwa baada ya Kamati ya Rufaa kuridhika na kuweka bayana kuwa
mwomba rufaa, Michael Richard Wambura aliipa Zabuni kampuni yake iitwayo
Min Investments & Commercial Services Co. wakati akiwa Katibu Mkuu wa FAT/TFF na hivyo kushindwa kukudhi kigezo cha uadilifu.
Katika kufikia maamuzi yake, Kamati ya rufaa pia ilibaini kuwa Ndg.
Michael Richard Wambura alionyesha kuwa alikuwa amechana na umiliki wa
kampuni hiyo kuanzia tarehe 12 Novemba 2003 kwa mabadiliko
yaliyotekelezwa tarehe 28 Februari 2007 kwa malipo ya Shs. 34,500/= ya “exchequer receipt No. 28173444’.
Hata hivyo, Kamati ya Rufaa iliridhika kuwa utekelezaji wa mabadiliko
ya umiliki wa kampuni hiyo ulichukua takribani miezi arobaini (40).
Baada ya majadiliano ambayo yalikuwa yamekitwa (pegged) kwenye uadilifu (integrity), Kamati ya Rufaa iliridhika kuwa taswira inayojitokeza kwenye muktadha imegubikwa na wingu jeusi la mashaka kuhusu “integrity” ya Muomba Rufaa (Ndg. Michael Richard Wambura).
Uthibitisho kwamba mmilki wa Kampuni ya Min Investments & Commercial Services Co
ni Ndg. Michael Richard Wambura ulitolewa na Msajili wa Makampuni
(Business Registration and Licensing Agency-BRELA) kwa barua yenye
Kumbukumbu Na. MITM/RBN/93017 ya tarehe 16 Agosti 2006. Kampuni hiyo
ilisajiliwa tarehe 17 Julai 1992.
Kamati ya Uchaguzi ya TFF inatoa sehemu ndogo tu ya ubadhirifu uliokuwa unafanywa kwa kutumia Kampuni hiyo (Min Investments & Commercial Services Co)
ya Michael Wambura kinyume na utaratibu wa utoaji tenda wa FAT/TFF na
malipo aliyojilipa bila maelezo yoyote kama ilivyoainishwa kwenye Ripoti
ya Ukaguzi wa Mahesabu iliyowasilishwa na wakaguzi tarehe 19 Septemba
2005 na Ripoti maalumu ya ukaguzi iliyowasilishwa Novemba 2006, kama
ifuatavyo:
(i) Tarehe
28 Julai 2004 Michael Wambura akiwa Katibu Mkuu wa TFF alilipwa Dola za
Kimarekani 16,548.00 (US$ 16,548 sawa na Tshs. 17,170,040 wakati huo)
kwa ununuzi wa samani (furniture) za Hosteli ya TFF. Pesa hizo
zilizoombwa kulipwa kwa Michael Wambura zimeonyeshwa kwenye fomu ya
malipo ya TFF ya tarehe 28 Julai 2004. Pesa hizo zilipokelewa na Kampuni
ya Min Investments & Commercial Services Co
na kuthibitisha kupokelewa na kampuni hiyo kwa risiti Na. 020 ya tarehe
21 Julai 2004 ya kampuni hiyo, ingawa hapakuwa na maombi ya manunuzi
(order) iliyokuwa imefanywa na TFF kwa kampuni hiyo.
(ii) Baada
ya kujilipa pesa zilizotajwa hapo juu, kesho yake tarehe 29 Julai 2004
Ndg. Michael Wambura akiwa Katibu Mkuu wa TFF alijilipa Dola za
kimarekani 25,000.00 (US$ 25,000.00 sawa na Tshs. 25,937,500 wakati
huo), kama ilivyoonyeshwa kwenye vocha ya malipo ya TFF Na. 5324 ya
tarehe tajwa hapo juu, ikionyesha kuwa ni kwa ajili ya malipo ya samani
za Hosteli (US$ 15,000.00) na malipo ya awali ya Gari (US$ 10,000.00).
Ndg. Michael Wambura alithibitisha kupokea malipo hayo. Ripoti ya
Ukaguzi inabainisha wazi kuwa vifaa vichache vilivyonuliwa kwa hosteli
ya TFF thamani yake haikuainishwa na hapakuwa na gari lililolipiwa
malipo ya awali katika vitabu vya mahesabu ya TFF.
(iii) Katika
kipindi cha mwaka 2002 Ndg. Michael Wambura akiwa Katibu Mkuu wa FAT
alijikopesha jumla ya Tshs. 36,850,750 bila idhini ya Kamati ya
Utendaji.
(iv) Tarehe 20 Mei 2002 Ndg. Michael Wambura akiwa Katibu Mkuu wa FAT alijilipa Tshs. 12,147,837 ambazo hazina maelezo yoyote.
(v) Imebainishwa
wazi kuwa FAT/TFF ilikuwa mfilisi katika kipindi cha 2002-2004 (Nukuu:
“The Association was actually insolvent during the period.”)
Kamati
inaweka wazi tena kwamba maamuzi yaliyofikiwa na Kamati ya Rufaa ya
kumuengua Michael Wambura kwenye uchaguzi Mkuu wa TFF yanaweza tu
kubadilishwa na Mahakama ya usuluhishi wa masuala ya michezo (CAS)
endapo Michael Wambura atakata rufaa CAS kupinga maamuzi hayo na
kushinda rufaa, na si vinginevyo.
MAAMUZI YA MKUTANO MKUU WA TFF 2007
Mkutano Mkuu wa TFF ambacho ndicho chombo cha juu kabisa cha TFF (Supreme Authority of TFF)
katika kikao chake mwaka 2007 kilipitia ripoti za ukaguzi wa mahesabu
ya FAT/TFF kwa kipindi cha mwaka 2002 hadi 2004 na baada ya kujiridhisha
kuhusu ubadhirifu uliofanywa na Ndg. Michael Wambura, Mkutano Muu wa
TFF uliamua kwamba Ndg.
Michael Wambura afikishwe kwenye vyombo vya dola kwa ubadhirifu wa
fedha za FAT/TFF alioufanya kama ilivyoainishwa kwenye ripoti za ukaguzi
wa Mahesabu. Sekretarieti ya TFF mwaka 2007 ikitekeleza maagizo ya
Mkutano Mkuu wa TFF na suala hilo lilpelekwa Jeshi la Polisi. Jeshi la Polisi ilithibitisha maombi ya TFF kwa barua yake ya tarehe 18 Januari 2008 na kumfungulia jalada Ndg Michael Wambura kwa kosa la wizi akiwa Mtumishi. Kamati ya Uchaguzi ya TFF inaheshimu maamuzi ya Mkutano Mkuu wa TFF na hadi sasa haijataarifiwa kwa maandishi na chombo chochote kama suala hilo limefikia ukomo wa aina yoyote.
UCHAGUZI WA KLABU YA SIMBA MWAKA 2010
Ndg.
Michael Richard Wambura aliomba kugombea nafasi ya Mwenyekiti wa Klabu
ya Simba. Hata hivyo alikatiwa rufaa na Ndg. Daniel T. Kamna kwa
kutotimiza matakwa ya Ibara ya 9 ya Kanuni za Uchaguzi za wanachama wa
TFF kama ilivyoamuliwa na Kamati ya Uchaguzi ya TFF na pia Kamati ya
Rufaa ya TFF mwaka 2008 wakati alipoomba kugombea nafasi ya Makamu wa
kwanza wa Rais wa TFF. Kamati ilikubaliana na maamuzi yaliyotolewa na
Kamati ya Uchaguzi na Kamati ya Rufaa ya TFF mwaka 2008 kwamba Bw.
Michael R. Wambura si mwadilifu kama
ilivyonyeshwa kwenye aya ya 2.1 na 2.2 hapo juu na hivyo hakukidhi
matakwa ya Ibara ya 29(7) ya Katiba ya TFF na Ibara ya 9 ya Kanuni za
Uchaguzi za wanachama wa TFF. Kamati ilimuondoa kugombea nafasi ya Mwenyekiti wa Simba SC.
Baada
ya maamuzi hayo ya Kamati, Ndg. Michael Richard Wambura alikwenda
Mahakamani na akafungua kesi kwenye Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, Dar es salaam
dhidi ya Mwenyekiti wa Klabu ya Simba kuzuia uchaguzi wa klabu ya Simba
usifanyike. Kwa kufanya hivyo alivunja Katiba ya Klabu ya Simba na
kukiuka Katiba ya TFF Ibara ya 12(2) (e) na Katiba ya FIFA Ibara ya
64(2). Klabu ya Simba ilichukua hatua za kikatiba, na katika kikao chake
cha 5/5/2010, ilimsimamisha uanachama Ndg. Wambura kwa kukiuka katiba
ya klabu hiyo. Klabu ya Simba iliitaarifu TFF uamuzi huo kwa barua yenye
Kumbukumbu Na. SSC/MMKT/162/Vol.40/10 ya tarehe 06 Mei 2010
iliyoambatanishwa na Muhtasari wa kikao cha Kamati ya Utendaji
kilichofanya uamuzi huo. Uamuzi wa kumrudishia uanachama unafanywa na
Mkutano Mkuu wa Klabu ya Simba. TFF haijapokea taarifa yoyote kutoka
Klabu ya Simba kwamba Mkutano Mkuu wa Klabu hiyo ulikwisha msamehe. Kwa
hali hiyo taarifa ya kusimamishwa kwake iliyotumwa TFF mwezi Mei 2010
itaendelea kuzingatiwa hadi hapo Klabu ya Simba itakapo ijulisha TFF
mabadiliko ya maamuzi hayo.
3. MAAMUZI KUHUSU UCHAGUZI WA FAM
Kamati
ya Uchaguzi ya TFF ilimuondoa Ndg. Michael Wambura kugombea nafasi ya
Mwenyekiti wa FAM kwa kuwa alifungua kesi kwenye Mahakama ya Hakimu
Mkazi Kisutu, Dar es salaam dhidi ya Mwenyekiti wa Klabu ya Simba akiwa
ni mwanachama wa Klabu ya Simba kuzuia uchaguzi wa klabu ya Simba
usifanyike, jambo ambalo ni uvunjaji wa Katiba ya Klabu ya Simba,
ukiukwaji wa Katiba ya FAM, TFF na FIFA.
Pia, Kamati ya Uchaguzi ya TFF iliweka wazi kama
ilivyobainisha kwenye uchaguzi wa Klabu ya Simba kwamba suala la
uadilifu wa Ndg. Wambura lilishafanyiwa maamuzi na Kamati ya Rufaa ya
TFF mwaka 2008 kwa mujibu wa Kanuni za Uchaguzi Mkuu wa TFF. Kwa mujibu
wa Kanuni za Uchaguzi huo na Katiba ya TFF Mamlaka pekee inayoweza
kutengua uamuzi huo ni Mahakama ya Usuluhishi wa masuala ya Michezo
(CAS) iliyo na makao yake Lausanne, Switzerland.
Baada
ya uamuzi huo, Kamati ya Uchaguzi ya TFF imeshuhudia baadhi ya vyombo
vya TFF vikishughulikia masuala ya uchaguzi kinyume na matakwa ya Katiba
ya TFF na Kanuni za Uchaguzi, kama ifuatavyo:
(i) Katika
hali isiyozingatia Kanuni za Uchaguzi za wanachama wa TFF, Kamati ya
Nidhamu ilipokea malalamiko ya Ndg. Michael Wambura yaliyoitwa ‘rufaa’.
Kwa kuwa hakuna utaratibu wa masuala ya uchaguzi kukatiwa rufaa kwenye
Kamati za nidhamu katika ngazi zote za uchaguzi na hivyo pia kutokuwepo
ada ya ‘rufaa’ za aina hiyo, mlalamikaji alilazimisha kupokelewa ada ya
Tshs 300,000/= ambayo ni ada inayotumika kwa rufaa za Ligi Kuu ya Vodacom ambayo imeainishwa katika Ibara ya 17 ya kanuni za mashindano hayo. Ada
hiyo iliwekwa (deposited) kwenye Akaunti ya TFF bila ridhaa ya TFF.
Pamoja na mapungufu hayo “rufaa’ hiyo ilisikilizwa na Kamati ya Nidhamu
na kutolewa maamuzi. Mlalamikaji hakuridhika na maamuzi ya Kamati hiyo
na aliamua kukata ‘rufaa’ katika Kamati ya Rufaa ya TFF.
(ii) Kamati
ya Rufaa ya TFF ilipokea na kusikiliza ‘rufaa’ ya Ndg. Michael Richard
Wambura, kinyume na matakwa ya Kanuni za Uchaguzi za wanachama wa TFF.
Kwa kuwa kwa mujibu wa Kanuni za Uchaguzi za wanachama wa TFF hakuna
rufaa inayokatwa kwenye Kamati hiyo, hivyo kutokuwapo ada yoyote kwa
“rufaa” ya aina hiyo, ili kutimiza azma ya kusikiliza ‘rufaa’ hiyo,
palifanyika juhudi za kulazimisha kupokelewa ‘ada’ ya Shilingi 500,000/=
ambayo ni ada ya rufaa za mashindano ya Ligi Kuu ya Vodacom ambayo
imeainishwa pia katika Ibara ya 17 ya kanuni za mashindano ya Ligi Kuu ya Vodacom. Hata hivyo, ada hiyo ambayo si halali, haikupokelwa na Sekretarieti ya TFF baada ya kushindikana kuainisha ada ya mashindano ya Ligi Kuu ya Vodacom na masuala ya Uchaguzi. Bila kuzingatia Kanuni za Uchaguzi za wanachama wa TFF na Katiba ya TFF Ibara ya 47(4) inayotamka na kuikataza Kamati ya Rufaa kusikiliza rufaa kwa mambo yaliyowekewa ukomo na Kanuni husika; Ibara hiyo inatamka; ‘The
Appeal Committee shall be responsible for hearing appeals against
decisions from the Disciplinary Committee that are not declared final by
relevant regulations as well as decision passed by the players’ Status
Committee concerning the eligibility of players for the teams’,
Kamati hiyo ilisikiliza malalamiko ya Ndg. Michael Richard Wambura na
kutoa uamuzi bila kuzingatia Kanuni za Uchaguzi za wanachama wa TFF
ambazo ni ‘relevant regulations’ na Ibara ya 12(4) ya Kanuni hizo
kutamka wazi kuwa; ‘The decisions of the TFF Elections Committee are final and conclusive and shall not be monitored by any other body’.
(iii) Kamati
ya Uchaguzi ya TFF inatamuka wazi kuwa utaratibu mzima uliotumika
kupokea rufaa hiyo toka Kamati ya Nidhamu hadi ya Kamati ya Rufaa
haukufanyika kwa mujibu wa taratibu za ukataji rufaa zilizoainishwa
kwenye Kanuni za Uchaguzi za wanachama wa TFF. Ukataji
rufaa huo uliongozwa zaidi na hila kuliko dhamira ya kuheshimu taratibu
zilizowekwa. Mbali na kutumia kanuni za Ligi kuu ya Vodacom kusikiliza
‘rufaa’ hizo, uthibitisho mwingine wa hila na ujanjaujanja ni pale
mlalamikaji alipokwenda kuweka kwenye akaunti ya TFF ada ya rufaa ya
mashindano ya Ligi Kuu ambayo haitambuliki kwa mujibu wa Kanuni za
Uchaguzi na kutumia vyombo vya habari kutangaza kitendo hicho, lakini
baada ya kutolewa maamuzi na Kamati ya Rufaa alienda kimya kimya TFF
kuchukua ada hiyo ambayo ni ya rufaa kwa mashindano ya Ligi kuu.
(iv) Kamati
ya Uchaguzi ya TFF, kwa mamlaka yaliyo kasimiwa kwake na Katiba ya TFF
Ibara ya 49(1) , Kanuni za Uchaguzi za TFF Ibara ya 6, Kanuni za
Uchaguzi za wanachama wa TFF Ibara ya 8(2), 10(6), 12(4) na 26(2), na
pia kwa mamlaka yaliyoainishwa katika Katiba za wanachama wa TFF kuhusu
uchaguzi, katika kikao chake kilichofanyika 03 Desemba 2011 iliamua na
inatamka wazi kuwa maamuzi yaliyofanywa na Kamati ya Rufaa ni BATILI kwa
kuwa hayakuzingatia Kanuni za Uchaguzi za wanachama wa TFF. Kamati ya
Uchaguzi ya TFF inaziagiza Kamati zote za Uchaguzi za wanachama wa TFF
na wanachama wao kuendelea kuzingatia Kanuni za Uchaguzi katika utendaji
wa kazi zao za kuendesha na kusimamia chaguzi zote za vyama vya mpira
wa miguu nchini, ikiwa ni pamoja na kutozingatia maamuzi yoyote ya
uchaguzi yatakayofanyika kinyume na Kanuni za Uchaguzi.
4. TAARIFA ZA UDANGANYIFU KUTOKA KWA BAADHI YA WAGOMBEA UONGOZI KWENYE VYAMA WANACHAMA WA TFF.
Kamati
ya Uchaguzi inapenda kuwakumbusha wadau wote wa soka wenye nia ya
kugombea uongozi TFF na vyama wanachama wa TFF kuwa kwa mujibu wa Kanuni
za Uchaguzi za TFF ibara ya 25(8) na Kanuni za Uchaguzi za wanachama wa
TFF Ibara ya 26(8) ni makosa kuwasilisha taarifa za udanganyifu kwenye Kamati ya Uchaguzi. Kanuni hizo zinatamka kuwa; During
the election process any person or member who contravenes this code or
provides false particulars or qualification, may be penalized to a fine
not exceeding five hundred thousand shillings or be barred to
participate in the election process for 2 years or for both a fine and
such barring, provided that the General Secretary lodges a complaint to
the TFF judicial organ for disciplinary action.
Kamati
imebaini kuwa baadhi ya wagombea walifanya udanganyifu kuhusu vyeti
halisi walivyowasilisha kwenye uchaguzi wa FAM na pia baadhi ya waombaji
uongozi katika uchaguzi wa klabu ya Villa. Kwa mfano mwombaji aliyeomba
kugombea nafasi ya Mwenyekiti wa Klabu ya Villa cheti chake cha Elimu
ya Msingi alichowasilisha kwenye Kamati ya Uchaguzi kina utata. Vyote
hivyo viko katika hatua za uhakiki kwenye mamlaka husika, uhakiki
utakapokamilika Kamati itachukua hatua kwa mujibu wa Kanuni tajwa hapo
juu.
Kamati
imebaini na kujiridhisha kuwa Ndg. Michael Wambura alitoa taarifa
zinazokinzana kwenye Kamati ya Uchaguzi kuhusu umri wake. Katika
Uchaguzi wa Klabu ya Simba mwaka 2010, aliwasilisha taarifa kwamba
amezaliwa mwaka 1967 lakini katika uchaguzi wa Chama cha Mpira wa Miguu
Mkoa wa Mara aliwasilisha taarifa kwamba alizaliwa mwaka 1965. Taarifa
za umri zinazokinzana za mwombaji uongozi zinashiria mashaka ya umakini
na uadilifu wa mgombea hasa ikizingatiwa kuwa nafasi ya uongozi ya
mwenyekiti kwa vyama wanachama wa TFF na Rais wa TFF zina ukomo wa wa umri. Kamati itachukua hatua zilizoainishwa kwenye Kanuni za Uchaguzi tajwa hapo juu.
5. KAULI ZENYE LENGO LA KUVURUGA CHAGUZI ZA WANACHAMA WA TFF.
Katika siku za karibuni Kamati ya Uchaguzi ya TFF imeshuhudia kauli amabazo si za kiwanamichezo zenye lengo la kuleta vurugu katika michakato ya Uchaguzi. Kwa mfano
kauli za kuwahamasisha wadau wa soka kwenda mahakamani kwa masuala ya
michezo, hususan, kupinga michakato ya uchaguzi ni uvunjaji wa Kanuni za
Uchaguzi na Katiba ya TFF na FIFA. Kamati inawataka wadau wote wa soka
kuheshimu na kuzingatia Kanuni na taratibu za uchaguzi na Katiba ya TFF,
vinginevyo Kamati haitasita kuchukua hatua stahiki kwa mujibu wa Kanuni
za Uchaguzi.
Deogratias J. Lyatto
MWENYEKITI
KAMATI YA UCHAGUZI
SHIRIKISHO LA MPIRA WA MIGUU TANZANIA
chanzo na Shaffi Dauda
chanzo na Shaffi Dauda
No comments:
Post a Comment