Mar 7, 2012

Waarabu wampoteza Mganga wa Yanga




Mwenyekiti wa Yanga, Llyod Nchunga akibadilishana mawazo na katibu mkuu wa klabu hiyo, Celestine Mwesigwa kwenye uwanja wa ndege wa kimataifa wa Cairo
MICHAEL MOMBURI, CAIRO
INACHEKESHA lakini inavutia kusikia, kuona na hata kusoma. Yanga na Zamalek wikiendi iliyopita zilikuwa zikipimana nguvu ndani na nje ya uwanja jijini Cairo, Misri, katika mchezo wa Ligi ya Mabingwa Afrika.

Yanga ilikuwa na mganga wake ambaye alitua Cairo kimyakimya na muda wote alikuwa bize na mambo yake kama walivyokuwa wenzake wa Zamalek.

Waganga wa Zamalek inadaiwa walikuwapo uwanjani kuanzia Alhamisi usiku Yanga ilipokuwa ikipasha mazoezi.
Awali waganga hao pia walikuja karibu na hoteli ya Holiday Express ilipofikia Yanga lakini wakazuiwa.

Lakini cha kuchekesha zaidi mtaalamu huyo wa Yanga alifanya mambo yake kwenye Uwanja wa Jeshi wa Misri, siku moja kabla ya mechi na kuchafua hali ya hewa uwanjani huku kila mchezaji akijiuliza kunani?

Viongozi wa Yanga walionekana kuzuga na kuwa mbali na mtaalamu wao muda mwingi ili kupoteza ushahidi.

Lakini ujanja wote wa mganga huo ukakoma Jumamosi iliyopita ambayo ilikuwa ni siku ya mechi. Mambo yalianza wakati msafara wa timu ulipotaka kuondoka hotelini kuelekea uwanjani.

Mtaalamu huo aliwatia Yanga hofu kubwa baada ya kutojulikana aliko kwani alitafutwa kila kona ili aingie kwenye gari la mbele lililobeba viongozi na waandishi wa habari. Hakuonekana wala kwenye simu hakuwa akipatikana.

Hatua hiyo iliwafanya baadhi ya wazito wa Yanga kubaki hotelini kumtafuta zaidi. Baadaye ikaja kugundulika kuwa alikuwa amepitiwa na usingizi mzito chumbani kwake.

Ndipo walipolazimika kubisha hodi kwenye mlango wa chumba hicho kwa muda mrefu, hadi mtaalamu huyo alipoamka.

Baada ya kuamka, haraka haraka akapiga sala zake kisha wakaanza safari ya kuelekea Uwanja wa Chuo cha Jeshi la Misri, Yanga ilipokuwa ikicheza na Zamalek kwenye mechi ya marudiano ya Ligi ya Mabingwa.

Mmoja wa viongozi waliokuwa kwenye msafara huo wa kumsaka, alidai kuwa mtaalamu huo alipitiwa kwa vile alikuwa hajui mechi ni saa ngapi inachezwa ingawa mwingine alikuwa akikejeli kwamba utaalamu wake umegongana na ule wa Zamalek.

Lakini mganga huyo alipandishwa gari lenye kasi kubwa ambalo liliwahi kufika uwanjani na kuwakuta wachezaji kabla hawajaingia vyumbani, aliingia nao na wanajeshi wanaolinda uwanjani hapo walionekana kumhisi, lakini hawakumfanya lolote.

Alikuwa mjanja na aliwazidi maarifa kila alipobaini wanataka kumzuia.

Ingawa wachezaji walijua kinachoendelea na kuuchuna, lakini kocha Kosta Papic alionekana kutofurahishwa na uwepo wa mtaalamu huyo. Hata hivyo naye hakuweza kumfanya lolote kwani alikuwa hakai sehemu moja muda mwingi.

Siku ya Ijumaa wakati wa usiku baada ya Yanga kutoka mazoezini, mtu mmoja raia wa Misri aliyekuwa amevalia kiutata utata, alionekana akiranda nje ya hoteli ya Yanga ambako kiongozi wa msafara wa Yanga, waliyepewa na Zamalek, akawaambia askari wasimruhusu kuingia ndani kuwabughudhi Yanga.

�Mzuie huyo asije kuharibu mambo hapa,� alisikika kiongozi huyo wa msafara aliyeagizwa na Zamalek kuiongoza Yanga.

Ingawa hakuna kiongozi yoyote wa Yanga aliyekuwa tayari kuzungumzia vituko hivyo, lakini baadhi ya wanachama wa Yanga waliokuwepo jijini hapa, walidai kuwa hata Zamalek walikuwa fiti kwenye mambo ya uganga ndiyo maana mganga wa Yanga akawa anapambana nao kwa nguvu huku wakidai wakati fulani walimzidi nguvu.

Hata wakati Yanga inaondoka kurudi Dar es Salaam, mtaalamu huyo wa Yanga alichelewa kwa vile alikuwa akipiga dua na habari za uhakika zinadai alikuwa anatupa mabaki ya utaalam wake kwenye Uwanja wa Ndege wa Cairo juzi Jumatatu usiku.

Soka la Afrika limekuwa likitawaliwa na imani za ushirikina kwa miaka mingi sasa lakini makocha hususani wa kigeni wamekuwa wakidai haisaidii kwani ni imani tu.

Kocha wa Ghana, Goran Stevanovic, amekiri hivi karibuni kuwa wachezaji wake wanalogana na ndiyo maana timu hiyo iliboronga kwenye fainali za Kombe la Mataifa ya Afrika.                               chanzo na mwanaspoti

No comments: