Ryan Giggs, alikuwa na usiku
wa aina yake baada ya kufanikiwa kujiwekea historia ya kuwa mchezaji
mwenye umri mkubwa zaidi kuwahi kufunga katika michuano ya klabu bingwa
Ulaya na kuisaidia klabu yake ya Manchester United kufanikiwa kupata
sare ya bao 1-1 dhidi ya Benfica ya Ureno.
Katika pambano hilo ambalo lilikuwa wazi
kwa timu zote huku yeyote kati ya timu hizo mbili akionekana angeweza
kuibuka na ushindi ndani ya dakika tisini za mchezo, wenyeji
walitangulia kufunga kupitia kwa Oscar Cardozo kunako dakika ya 24 ya
mchezo.
Alifunga bao hilo baada ya kutumia
makosa ya mabeki wa United, ambapo aliachia shuti kali la umbali wa
takriban mita 18 hivi lililomshinda mlinda mlango wa United na baada ya
hapo wenyeji wakaonekana kama wangeongeza bao wakati wowote.
Hata hivyo, dakika chache kabla ya
mapumziko, Ryan Giggs alipokea pasi safi toka wingi ya kulia mwa uwanja
kabla ya kukokota mpira huku akiwadhibiti mabeki kadhaa wa Benfica na
kisha kuachia mkwaju safi na kuandika bao la kusawazisha, na matokeo
hayo yakasimama hivyo hadi wakati wa mapumziko.
Kipindi cha pili kilishuhudia timu zote
zikifanya mabadiliko kadhaa sanjari na kucheza kandanda safi lakini
zaidi ya kosakosa kadhaa kwa kila upande, hakuna timu iliyoweza kuliona
lango la mwenzie na hivyo hadi mwisho wa mchezo Benfica 1-1 United.
Bao la Giggs linamfanya aweke rekodi ya
kuwa mchezaji mkongwe zaidi kufunga katika michuano hiyo akiwa na umri
wa miaka 37 na siku 289, ambapo pia anampita mkongwe Raul Gonzalez kwa
kuwa mchezaji aliyefunga katika misimu mingi zaidi ya michuano hiyo,
akiwa amefikisha misimu 16 hivi sasa.
Wakati United wakiambulia sare ya
ugenini, jirani zao Manchester City nao walijikuta wakiambulia sare ya
nyumbani dhidi ya Napoli kwenye mechi ambayo wageni Napoli walitangulia
kufunga kupitia kwa Edinson Cavani lakini wenyeji wakajitutumua na
kusawazisha kupitia kwa Aleksander Kolarov dakika chache baadae.
Kule nchini Uholanzi, Ajax walibanwa
vilivyo na waliokuwa wageni wao Lyon ya kutokea nchini Ufaransa na
kuambulia sare ya bila kufungana lakini miamba ya Hispania Real Madrid
wakianza michuano hiyo vyema baada ya kuchomoza na ushindi wa bao 1-0 wa
ugenini kwenye uwanja wa Dinamo Zagreb, bao pekee la mchezo huo
likiwekwa kimiani na Angel Di Maria.
Mechi zingine za usiku huu zimeshuhudia
FC Basle wakiibuka na ushindi wa bao 2-1 dhidi ya SC Otelul Galati, huku
Inter Milan wakianza vibaya baada ya kukubali kichapo cha nyumbani cha
bao 1-0 toka kwa Trabzonspor.
Nao wafaransa Lille wakiwa nyumbani
wakaambulia sare ya bao 2-2 dhidi ya CSKA Moscow Ilhali Villarreal
wakiwaruhusu wageni wao Bayern Munich kuwaadhiri nyumbani kwa kichapo
cha bao 2-0
No comments:
Post a Comment