Nov 5, 2011

Yanga yavunja rekodi

MASOUD MASASI, Dodoma
YANGA imeweka rekodi mpya ya mapato katika Uwanja wa Jamhuri mjini Dodoma, baada ya kuingiza mapato ya Sh. 28.52 milioni kwenye mechi yake na Polisi Tanzania.
Katika mchezo huo uliofanyika Jumatano iliyopita, Yanga iliibuka na ushindi wa bao 1-0.

Mapato hayo ni rekodi kwani tangu kujengwa uwanja huo mwaka 1977, haujawahi kuingiza fedha nyingi kiasi hicho.
Yanga pia imevunja yake rekodi yake yenyewe kwenye uwanja huo, kwani msimu uliopita ilipocheza na timu hiyo, mapato yalikuwa kiasi cha Sh. 20 milioni.

Watani wao wa jadi, Simba, msimu uliopita iliingiza Sh.19.3 milioni katika pambano lililochezwa katika uwanja huo. Simba ilishinda mabao 2-0.

Akizungumza na Mwanaspoti, Katibu Mkuu wa Chama cha Soka Mkoa wa Dodoma (DOREFA), Abubakar Ibrahim, alisema katika mchezo huo kiingilio kilikuwa Sh. 5,000 kwa Jukwaa Kuu na mzunguko ilikuwa Sh. 3,000. Watazamaji 7,525 waliingia uwanjani.

Bao la Yanga katika mchezo huo lilipatikana dakika ya 44 kupitia kwa mshambuliaji wake Keneth Asamoah aliyemalizia pasi ya Hamisi Kiiza.chanzo na http://www.mwanaspoti.co.tz

No comments: